Tanzania na Nchi ya Falme za Kiarabu zimekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika masuala ya usalama wa eneo la Ghuba na bahari ya Hindi pia kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika nchi za Somalia na Sudan.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
Katika Mazungumzo hayo wawili hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha udugu wa muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili ikiwa ni pamoja na kufufua mazungumzo ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) ambayo kwa mara ya mwisho yalifanyika katika Mji wa Abu Dhabikatika Umoja wa Falme za Kiarabu ili kufufua na kutekeleza makubaliano ikiwa ni pamoja na kuangalia fursa za kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.