Tanzania itashiriki Maonesho ya Dunia ya Biashara (Expo 2020 yatakayofanyika Dubai kuanzia mwezi Oktoba 2020 na kumalizika mwezi April 2021.

Uwekaji saini wa Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho hayo ulifanywa tarehe 16 Januari 2019 na Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk.

Kwa upande wa UAE, mkataba huo uliwekwa saini na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo, Mhe. Balozi Mbarouk alieleza kuwa Serikali inayapa umuhimu mkubwa maonesho hayo kwa kuwa ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kwenye sekta za uwekezaji, biashara, viwanda, utalii na mila na utamaduni.

Aidha, Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020 alieleza kuwa amefurahishwa na hatua ya Tanzania kusaini Mkataba huo ambapo itatoa fursa kwa nchi kujiandaa mapema na taratibu nyingine za ushiriki.

Baada ya uwekaji saini wa Mkataba huo,` kitakachofuata ni utayarishaji wa simulizi ya maudhui ya maonesho (pitch story) ambayo inatakiwa kuthibitishwa na Kamati ya Kitaifa ya Tanzania ya DUBAI Expo 2020. Simulizi ya maudhui hayo yatahusu vipaumbele vya Tanzania kama vile maendeleo ya viwanda, miundombinu, masuala ya biashara na uwekezaji, utalii, kilimo, elimu, afya, sanaa na utamaduni. Simulizi ya maudhui pia itatumika katika kusanifu muonekana wa banda la maonesho la Tanzania.

Tanzania inakuwa miongozi mwa nchi washiriki zipatazo 100 ambazo tayari zimesaini Mkataba wa Ushiriki tangu Dubai ilipochaguliwa kuwa mwenyeji wa maonensho hayo.Wengine walioshuhudia uwekaji saini wa Mkataba huo ni Bw. Ali Jabir Mwadini, Kansela Mkuu, Ubalozi Mdogo wa Tanzania, Dubai; Bi Samira Ahmed Diria, Afisa Ubalozi; na kwa upande wa DUBAI EXPO 2020 ni Bi Manuela Garcia Pascual, Mkurugenzi wa Washiriki wa Kimataifa na Bi. Esther Omondi, Meneja wa Nchi/Afisa dawati la Tanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Dodoma.
17 Januari 2019

  • Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakiweka saini Mkataba wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Dunia (Dubai Expo 2020. Uwekaji saini huo ulifanyika Dubai jana Januari 16, 2019.
  • Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakionesha Mkataba mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.
  • Balozi wa Tanzania nchini UAE ambaye pia ni Kamishna Mkuu wa Tanzania wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk (kushoto) na Mkurugenzi wa DUBAI EXPO 2020, Mhe. Najeeb Mohammed Al Ali wakibadilishana mawazo mara baada ya zoezi la kuweka saini kukamilika.