Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi alipokutana na Waziri mweza wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Reem Al Hashimy huko Abu Dhabi

Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimekubaliana kuitisha haraka mkutano wa tume ya pamoja (JPC) ili kuendeleza ushirikiano baina yao katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi na kiusalama katika ukanda wa bahari ya Hindi.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo yaliyofanyika mjini Abu Dhabi baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Reem Al Hashimy.

Akizungumza mara baada ya mkutano wao huo, Waziri Reem Al Hashimy amesema Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zina mahusiano ya kipekee na ya kihistoria na kwamba amefurahishwa na ziara ya Prof. Kabudi na kwamba ziara hiyo itatoa fursa ya kujifunza zaidi katika nyanja za uwekezaji, utalii na biashara kwa kufuata sera imara na nzuri za Rais John Magufuli za kutaka kuiona Tanzania ikipiga hatua za kimaendeleo kama ilivyo kwa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Baada ya mazungumzo hayo Waziri Kabudi amesema, ziara yake imekuwa na manufaa katika Umoja wa Falme hizo za Kiarabu kwa kuwa imefungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara pamoja na kudumisha mahusiano mema baina ya nchi hizo.

Ameongeza kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu umeialika Tanzania kushirikia maonesho makubwa ya kimataifa ya kibiashara yajulikanayo kama  Expo 2020,ambapo Tanzania imepata fursa ya kushiriki katika nyanja ya uwezeshaji na italenga zaidi katika teknolojia mpya ya ulimwengu ujao hususani katika miundombinu, biashara na utalii ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amehitimisha ziara yake ya takribani siku kumi katika Nchi za China na Umoja wa Falme za Kiarabu.